Kuku alitokana na jamii ya kuku-mwitu
mwekundu wa Asia. Muda si muda, mwanadamu alitambua kwamba kuku anaweza
kufugwa kwa urahisi. Inashangaza kwamba miaka 2,000 hivi iliyopita,
Yesu Kristo alizungumzia jinsi kuku anavyokusanya vifaranga vyake na
kuvilinda chini ya mabawa yake. (Mathayo 23:37; 26:34)
Mfano huo unaonyesha kwamba kwa ujumla watu walimfahamu sana ndege
huyo. Lakini kuku walianza kufugwa kwa wingi na mayai kutagwa kwa
minajili ya biashara katika karne ya 19.
Leo nyama ya kuku inapendwa sana
kuliko nyama ya ndege mwingine yeyote. Kuku hufugwa na mamilioni ya
watu—hata wale wanaoishi mijini—kwa ajili ya chakula na biashara. Kwa
kweli, ni wanyama wachache sana wa kufugwa wanaoweza kusitawi katika
maeneo mbalimbali kama kuku. Nchi mbalimbali zimekuza kuku wa jamii
fulani ambao wanaweza kukidhi mahitaji yao na kustahimili hali ya hewa
ya sehemu hizo. Baadhi ya jamii hizo ni: kuku wa Australorp kutoka Australia; kuku ajulikanaye sana wa Leghorn, asili yake ni Mediterania lakini anapendwa sana nchini Marekani; kuku wa New Hampshire, kuku wa Plymouth Rock, kuku wa Rhode Island Red, na Wyandotte, kuku hao wanatoka Marekani; na Cornish, Orpington, na Sussex, wanatoka Uingereza.
Sayansi ya kisasa imefanya ufugaji wa
kuku uwe mojawapo ya utendaji wenye faida sana katika kilimo. Nchini
Marekani, wakulima hutumia mbinu bora za ulishaji na ufugaji. Wao pia
hudhibiti magonjwa ya kuku kwa njia za kisayansi. Watu wengi hushutumu
mbinu hizo za kisayansi za kuzalisha kuku wengi kuwa za ukatili. Lakini
licha ya shutuma hiyo wakulima wangali wanabuni njia bora zaidi za
kufuga ndege hao. Hivi sasa mtu mmoja tu anaweza kutunza kuku 25,000
hadi 50,000 akitumia mbinu za kisasa. Ndege hao huwa wamefikia uzani wa
kutosha kuuzwa sokoni baada ya miezi mitatu tu.*
Chanzo cha Nyama
Waweza kuona nyama ya kuku ikiuzwa
karibu kila mahali, iwe hotelini, mkahawani, au kwenye soko la nyama na
vinywaji. Kwa kweli, mikahawa mingi ulimwenguni pote huuza hasa kuku.
Jamii fulani hupika nyama ya kuku kunapokuwa na sherehe za pekee. Na
katika baadhi ya nchi, kama vile India, mapishi mbalimbali ya kuvutia ya
kuku yamebuniwa. Mapishi kama vile lal murgi, kuku aliyepikwa kwa pilipili-hoho; kurgi murgi, kuku aliyechanwa; na adrak murgi, kuku aliyepikwa kwa mchuzi wa tangawizi, huwa na ladha sana!
Mbona kuku wanapendwa sana? Kwanza,
ni vyakula vichache tu vinavyoweza kutayarishwa kwa kutumia vikolezo
mbalimbali. Wewe hupenda kuku aliyepikwaje? Je, unapenda kuku
aliyekaangwa, aliyechomwa, aliyebanikwa, aliyepikwa kwa mvuke, au
aliyechemshwa polepole? Ukitazama kitabu chochote cha mapishi huenda
ukaona mapishi mengi sana ya kuku yanayokusudiwa kuboresha ladha ya
kuku.
Kuku huuzwa kwa bei nafuu pia kwa
sababu wanapatikana katika nchi nyingi. Wataalamu wa lishe hupendekeza
nyama ya kuku, kwa sababu ina protini, vitamini, na madini ambayo ni
muhimu kwa afya. Na bado, nyama ya kuku ina kalori chache, asidi-mafuta chache, na mafuta mengine.
Kulisha Nchi Zinazositawi
Bila shaka, nchi nyingine hazina
bidhaa tele za kuku. Jambo hilo lapasa kufikiriwa kwa sababu ripoti ya
tume maalumu ya Baraza la Sayansi ya Kilimo na Tekinolojia, ilisema
hivi: “Idadi ya watu ulimwenguni inatarajiwa kuongezeka kufikia bilioni
7.7 mwaka wa 2020 . . . Hata hivyo, sehemu kubwa (asilimia 95) ya
ongezeko hilo inatarajiwa kutukia katika nchi zinazositawi.” Taarifa
hiyo inatisha zaidi unapofikiria kwamba tayari watu wapatao milioni 800
wana utapiamlo!
Hata hivyo, wataalamu wengi wanaona
kwamba kuku wanaweza kutumiwa kulisha watu hao wenye njaa na wakulima
wanaweza kupata riziki kwa kuuza kuku. Tatizo ni kwamba si rahisi kwa
wakulima maskini kufuga kuku wengi sana. Jambo la kwanza ni kwamba
katika nchi maskini kuku hufugwa hasa kwenye mashamba madogo vijijini,
au katika vizimba vidogo. Na katika nchi hizo, kwa kawaida kuku
hawatunzwi katika mazingira salama. Wakati wa mchana kuku huachiliwa ili
wazurure-zurure ovyo na kutafuta chakula, kisha hurejea nyumbani usiku,
nyakati nyingine wanalala mitini au katika vizimba vya mabati.
Si ajabu kwamba kuku wengi wanaotunzwa hivyo hufa—baadhi yao kutokana na ugonjwa hatari wa Newcastle na
wengine huuawa na wanyama na wanadamu. Wakulima wengi hawana ujuzi wala
uwezo wa kulisha kuku wao ifaavyo, hawawezi kuwatengenezea makao
yafaayo, au kuwalinda na magonjwa. Ndiyo sababu miradi ya kuwaelimisha
wakulima katika nchi zinazositawi imeanzishwa. Kwa mfano, Shirika la
Umoja wa Mataifa la Chakula na Kilimo, hivi majuzi lilianzisha mradi wa
miaka mitano wa “kuwasaidia wakazi maskini wa Afrika wanaoishi
mashambani kupitia ufugaji wa kuku.”
Tungali twasubiri kuona matokeo ya
jitihada hizo nzuri. Basi ni jambo lifaalo kwa wakazi wa nchi tajiri
kutambua kwamba mlo wanaoona kuwa wa kawaida kwao kama vile kipande cha
kuku yamkini ni mlo ghali sana kwa watu wengi duniani. Kwa watu hao,
kula kuku ni kama ndoto tu.
WASILIANA NASI KWA;
0745 101842
hwilliady@ymail.com
WASILIANA NASI KWA;
0745 101842
hwilliady@ymail.com
No comments:
Post a Comment